UJASIRIAMALI

Ugumu wa kupata Mitaji

Wajasiriamali wamejikuta katika matatizo ya kubeba mizigo ya madeni kiasi cha kushindwa kuendelea

Nini maana ya mtaji?

Watu wengi wanaufahamu "Mtaji"  kwa lugha rahisi kama "Kianzio" cha biashara. Ni kweli, kwa mfano mtaji wa mama Ntilie ni Maji, sufuria, jiko, mkaa, mwiko, sahani, pamoja na fedha ya kununulia chakula kama mchele, nyanya, maharage, chumvi n.k.
Sasa basi katika mtiririko wa mahitaji yaliyotajwa hapo, vyote vinahitaji pesa ili kuvipata.

Tatizo liko wapi?

Kupata mtaji kwa nyakati hizi imekuwa jambo linalosumbua watu wengi. Mabenki yanasita kukopesha wafanya biashara wadogo sana (Micro businesses) kutokana na sababu kadha wa kadha ambazo kwayo ukiangalia zina uzito. Kada hii ya wafanya biashara huwa hawaaminiki kwa wakopaji wakubwa kama mabenki na taasisi za fedha kutokana na sababu zifuatazo: Hawana ofisi za kudumu; Wanakosa  dhamana n.k

Kupata fedha za kuanzisha biashara imekuwa ni kama ndoto!!


Suala la upatikanaji wa mtaji umeelezwa na wajasiriamali wengi kuwa kikwazo kikubwa na kinachozuia wajasiriamali wapya kungia kwenye sekta hii. Wanajiuliza: je, ni wapi watapata fedha?

“Ukosefu wa fedha wa kuanzisha biashara” umeelezwa kuwa dalili mbaya ya tatizo linalozuia maendeleo ya wajasiriamali. Unahitajika ufumbuzi wa haraka ili kumkomboa mfanyabiashara mdogo. 

Wakati mwingine tatizo la upatikanaji wa mitaji unasababishwa na mabenki kukosa Sera za ukopeshaji zitakazowanufaisha wafanyabiashara wadogo kwa kuweka masharti magumu yasiyotekelezeka. Kwa mfano:

·  Kiasi cha juu cha kukopesha huwa ni kidogo sana kuweza kukidhi mahitaji;

·   Mikopo hutolewa mijini tu, na kuacha sehemu kubwa ya wananchi wanaoishi vijijini kukosa fursa hii

·  Maombi ya mkopo huambatana na taratibu ngumu kama kuwa na Leseni za biashara, TIN namba kutoka TRA n.k (Mfano: Muuzaji wa genge hana elimu ya Kodi hivyo haoni sababu ya kuwa na vitu hivyo).

Pia Ukosekanaji wa Vitambulisho vya kitaifa (Inawia vigumu kwa Mabenki kumtafuta mkopaji).


Mabenki na Wakopeshaji wanasemaje?

Kwa upande wa Mabenki na wakopeshaji nao wanajitetea kuwa sio rahisi kutoa mkopo kwa mjasiriamali mdogo kutokana na sababu zifuatazo:-

·  Hurka wa watanzania katika kukwepa kulipa madeni

·  Wajasiriamali wengi kukosa ofisi za kudumu na zinazotambulika kisheria

·  Upungufu uliopo kwenye sheria ya nchi unaomlinda zaidi mkopaji aliyeshindwa kulipa deni na “kutomjali’ mkopaji

·  Wajasiriamali kukosa dhamana zenye kutambulika (mfano; mali zisizohamishika kama Hati za nyumba zilizosajiliwa).

·  Ukosefu wa elimu ya utunzaji wa mahesabu

·  Wajasiriamali wanakosa miradi ya maendeleo inayosababishwa na kokosa ujuzi wa kufanya michanganua ya biasharazao.

Umuhimu wa wajasiriamali wadogo wadogo sana


Hapa ninazungumzia kada ya wafanya biashara ambao mitaji yao haizidi TZS 5.0 million, ambayo mara nyingi huweza kuajili watu wasiozidi wanne na iwapo itatokea akafanya biashara mzunguko wake wa mauzo hauzidi TZS 12.0 million.

Mfano wa biashara zinazoangukia kwenye kada hii ni Ufugaji wa kuku, Mama Lishe, Useremala, Machinga, Wauzaji wa magenge na nyingine nyingi. 
Ni ukweli usio pingika kuwa jamii hii ya wajasiriamali wadogo pamoja na wale wa kati wanatoa mchango mkubwa katika mikakati ya Serikali ya kukuza uchumi na kupunguza Umaskini (MKUKUTA) kwa Tanzania Bara na Mpango wa Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA).


Kwa kuelewa umuhimu huu, blog ya Mjasiria-mali imeamua kutoa elimu kwa ufupi kuhusu ujasiriamali mahususi kwa wafanya biashara wadogo wadogo sana (Micro businesses) ili kuwawezesha kutambua mbinu mbalimbali za kukuza, kuimarisha na kudumu katika biashara.

Kumbukumbu zimeonyesha kuwa sekta ya Ujasiriamali kwa ujumla wake imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya  nchi kama ifuatavyo:
  • Kuongeza kipato na Ajira: hususan kipindi hiki ambacho kuna uhaba wa ajira za maofisini; watu wamekuwa wanajiajiri wenyewe  kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo kama tnavyoshuhudia utitiri wa vibanda vya mawakala wa M-pesa, Tigo Pesa, ‘stationary', maduka ya chakula n.k
  • Ni chanzo kikuu cha bidhaa na huduma mbalimbali: Mifano ni bidhaa za chakula, uchongaji n.k 
  • Imechangia 50% ya Pato la Taifa
  • Imechangia kuongezeka kwa idadi ya wajasiriamali. 




Maana ya Ujasiriamali


Ujasiriamali ni kitendo cha kuwa na tabia ya "Uthubutu". Hii tunaweza kuufananisha na uwezo (fursa) wa kutafuta masoko na kubuni vyanzo vipya vya biashara (Opportunities) ili mradi kuweza kuzalisha mali ama kutoa huduma itakayopelekea kuongeza kipato. 


Hata hivyo yote haya yanahitaji muda, fedha na juhudi binafsi (Hii ni sawa na ile dhana inayojulikana kama: "Mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe").


Sifa za Mjasiariamali

Ni mtafutaji Jasiri, anayethubutu kuamua kufanya biashara, mwenye uwezo wa kutambua mapema fursa mbalimbali za biashara, kukabiliana na vikwazo, na kutengeneza faida ya biashara hiyo. 

Ujasiriamali ni sawa na usanii ambao ni lazima uingie ucheze sehemu yako mwenyewe. Mara nyingi bila kuwapo usimamizi wa biashara na uwepo wako unaweza kupoteza mwelekeo.



Karibuni Mjasiriamali Blog


Karibuni tujumuike pamoja kupata habari za Kiuchumi na Ujasiliamali hususani katika sekta wa wafanya biashara wadogo wadogo sana (Micro business) katika kutoa elimu ya Ujasiriamali (Entrepreneurial skills) nchini Tanzania.
Hakika kuelimishana au kukumbushana mambo mbalimbali juu ya ujasiriamali hapa Tanzania kutaweza kutusaidia kuongeza ujuzi na kuongeza ufanisi wa biashara na kutoa fursa kwa wajasiliamali wapya kufahamu "ABC" za sekta hii muhimu katika kukuza uchumi wa nchi yetu.

Nia ni kutoa maelezo kwa ufupi kuhusiana na dhana ya ujasiriamali, matokeo mazuri ya kutoa elimu ya ujasiriamali kama vile kukuza biashara; kuongeza kipato na kupunguza umaskini katika jamii ya mtanzania; na kuongeza mapato ya Serikali kwa ujumla.

Wajasiriamali wengi wanahitaji elimu katika mambo yafuatayo:-
  • Ufahamu wa mikakati ya mbinu za kukuza biashara;
  • Kujua mikakati ya kukabiliana na ushindani wamasoko;
  • Uelewa wa namna ya kumjali na kuvuta wateja; na
  • Ufahamu wa jinsi ya kuandaa na kutunza kumbukumbu za biashara zao.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Jifunze ujasiriamali